MBIO za usajili zinaendelea huku kukiwa na ‘sarakasi’ nyingi kila timu ikijiweka sawa kwa msimu ujao, Simba, juzi ilifanikiwa kuipiku Yanga baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji wawili ambao walikuwa wakiwaniwa na watani wao wa jadi.
Wachezaji hao ni mabeki Haji Nuhu aliyekuwa Azam FC ambapo amesaini mkataba wa mwaka mmoja na Mohammed Fakhi wa JKT Ruvu aliyepewa mkataba wa miaka miwili.Wakizungumza na Championi Ijumaa kwa nyakati tofauti, wachezaji hao walifunguka jinsi walivyokuwa wakitegemea kuvaa uzi wa njano na kijani msimu ujao lakini ghafla wakadondokea Msimbazi.
“Sikujua lolote kuhusu kucheza Simba kwa kuwa nilikuwa nafanya mazungumzo na Yanga kwa kipindi chote lakini jana (juzi) asubuhi viongozi wa Simba walinipigia simu na kunitaka nifike Dar,” alisema Nuhu anayemudu kucheza beki ya kushoto na kuongeza:
“Nilipofika tukazungumza na kukubaliana kila kitu siku hiyohiyo, nikasaini kisha nikarudi nyumbani Zanzibar. Kuhusiana na ushindani wa namba naamini nitapata namba kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu namjua vizuri Tshabalala (Mohammed Hussein).”
Upande wa Fakhi anayemudu kucheza beki ya kati alisema: “Nilizungumza na klabu zote mbili lakini nilijua nitatua Yanga, kwa kuwa nilimalizana nao kwa asilimia kubwa lakini wakati wao wakizubaa Simba wakaja, nikazungumza nao kila kitu tukakubaliana nikasaini.”
BOFYA HAPA KWA KUJIUNGA NASI MOJA KWA MOJA NA LIKE PAGE YETU
HII NI MO DESIGN

Post a Comment